Ijumaa. 10 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 15 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 17, 2017)  

Somo la 1

Kut. 1:8-14,22

Aliinuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi, tena wana nguvu kuliko sisi. Haya! na tuwatendee kwa akili, wasije wakaongezeka; tena, kukitokea vita, wao nao wasije wakashikamana na adui zetu na kupigana nasi, na kutoka katika nchi hii, Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. Lakini kwa kadiri ya walivyowatesa ndivyo walivyoongezeka na kuzidi kuenea. Nao walichukiwa kwa sababu ya wana wa Israeli. Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. Kisha huyo Farao akawaagiza watu wake, akisema, Kila mtoto mwanamume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtahifadhi hai

Wimbo wa Katikati

Zab. 124

Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi
wanadamu walipotushambulia.
Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu.
Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu
Maji yafurikayo.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Na ahimidiwe Bwana:
Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno hayo.
Nafsi yetu imeokoka kama ndege
Katika mtego wa wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
(K) Msaade wetu u katika jina la Bwana.

Shangilio

1 Sam. 3:9 Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia:
wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Injili

Mt. 10:34 - 11:l

Yesu aliwafundisha mitume wake: Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! sikuja kuleta amani, bali upanga. Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu; na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake. Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipomimi, ampokea yeye aliyenituma. Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki. Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake. Ikawa Yesu alipokwisha kuwaagiza wanafunzi wake kumi na wawili, alitoka huko kwenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao.

Maoni


Ingia utoe maoni