Jumatatu. 20 Mei. 2024

Masomo ya Misa

DOMINIKA YA 14 YA MWAKA (Jumapili, Julai 09, 2017)  

Somo la 1

Zek. 9:9-10

Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za Amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.

Wimbo wa Katikati

Zab. 145:1-2, 8-11, 14, 17

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako.
(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.


Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zako zote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini.
(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.

Somo la 2

Rum. 8:9, 11-13

Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili; kwa maana kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

Shangilio

1Sam. 3:9; Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia;
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Injili

Mt. 11:25 – 30

Wakati ule Yesu alijibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kuwa kwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

Maoni


Ingia utoe maoni