Jumatatu. 20 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 13 ya Mwaka (Alhamisi, Julai 06, 2017)  

Somo la 1

Mwa 22:1-19

Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu. Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali. Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na Kuwarudia tena. Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja, Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babaangu! Naye akasema, Mimi hapa mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo,lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi waka endelea wote wawili pamoja. Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinge mwanawe. Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana; mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana; sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pemba zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa Bwana itapatikana. Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu pili kutoka mbinguni, akasema, Nimeapa kwa nafasi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda nenno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kumilikizidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umeti sauti yangu. Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

Wimbo wa Katikati

Zab. 116 :1-6, 8-9

Aleluya.
Nampenda Bwana kwa kuwa anaisikiliza
Sauti yangu na dua zangu
Kwa maana amenitegea sikio lake,
Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai

Kamba za mauti zilinizunguka,
Shida za kuzimu zilinipata.
Naliona taabu na huzuni;
N’ikaliitia jina la Bwana.
Ee Bwana, nakuomba sana,
Uniokoe nafsi yangu.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai

Bwana huwalinda wasio na hila;
Naliadhilika, akaniokoa.
Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako,
Kwa kuwa Bwana amekutenda ukarimu.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai

Maana umeniponya nafsi yangu na mauti,
Macho yangu na machozi,
Na miguu yangu na kuanguka.
Nitaenenda mbele za Bwana
Katika nchi za walio hai.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana katika nchi za walio hai

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Mbegu ni neno la Mungu,
anayepanda ni Kristo.
atakayemkuta, ataishi milele.
Aleluya.

Injili

Mt. 9:1-8

Yesu alipanda chomboni, akavuka, akafika mjini kwao. Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye Yesu, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu; umesamehewa dhambi zako. Na tazama. Baadhi ya waandishi wakasema nafsini mwao, Huyu anakufuru. Naye Yesu hali akijua mawazo yao, akasema, Mbona mnawaza maovu mioyoni mwenu? Kwa maana rahisi ni lipi, ni kusema, Umesamehewa dhambi zako, au ni kusema, Ondoka, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (amwambia yule mwenye kupooza) Ondoka, ujitwike kitanda chako, uende nyumbani kwako. Akaondoka, akaenda zake nyumbani kwake. Makutano walipomwona, walishikwa na hofu, wakamtukuza Mungu, aliyewapa watu amri ya namna hii.

Maoni


Ingia utoe maoni