Jumatatu. 20 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 12 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 30, 2017)  

Somo la 1

Mwa 17:1,9-10,15-22

Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume na kwenu atatahiriwa. Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema movoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako. Mungu akasema, sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu. Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao. Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 128 : 1-5

Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika nyia yake.
(K) Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana.

Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao.
Wanao Kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako.
(K) Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana.

Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Hone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako.
(K) Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana.

Shangilio

MT 11:25

Aleluya, Aleluya,
Nashukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi,
kwa kuwa mambo haya uliwaficha
wenye hekima na akili, ukawafunulia
watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Mt. 8:1-4

Yesu aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.

Maoni


Ingia utoe maoni