Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU IRENEO, ASKOFU NA MSHAHIDI (Jumatano, Juni 28, 2017)  

Somo la 1

Mwa 15: 1-12, 17-18

Neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana Mungu, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, Na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akawaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati.

Wimbo wa Katikati

Zab. 105:1-4,6-9 (K)

Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake,
Wajulisheni watu matendo yake,
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,
Zitafakarini ajabu zake zote.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

Jisifuni kwa jina lake takatifu,
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana.
Mtakeni Bwana na nguvu zake,
Utafuteni uso wake sikuzote.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.


Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
Duniani mwote mna hukumu zake.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.


Analikumbuka agano lake milele;
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
Agano alilofanya na Ibrahimu,
uapo wake kwa Isaka.
(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

Shangilio

Zab. 147 : 12, 15

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.

Injili

Mt 7:15-20

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.

Maoni


Ingia utoe maoni