Jumatatu. 16 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumapili ya 5 ya Kwaresima (Jumapili, Machi 13, 2016)  

Somo la 1

Isa 43: 16-21

Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi. Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

Wimbo wa Katikati

Zab 126

Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni, Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, Na ulimi wetu kelele za furaha.
(K)Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.

Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.
(K)Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.

Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha.
(K)Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.

Ingawa mtu anakwenda zake akilia, Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha, Aichukuapo miganda yake.
(K)Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.

Somo la 2

Flp 3:8-14

Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.

Injili

Yn 8:1-11

Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.

Maoni


Ingia utoe maoni