Jumapili. 12 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 4 ya Kwaresima (Jumamosi, Machi 12, 2016)  

Somo la 1

Yer 11:18-20

Tena Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Wimbo wa Katikati

Zab 7:1-2, 8-12



Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama simba, Akiivunja-vunja pasipokuwa na wa kuponya.
(K)Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia wewe.

Bwana, unihukumu mimi, Kwa kadiri ya haki yangu, Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki.
(K)Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia wewe.

Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.
Mtu asiporejea ataunoa upanga wake; Ameupinda uta wake na kuuweka tayari
(K)Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia wewe.

Injili

Yn 7:40-52

Basi wengine katika mkutano walipoyasikia maneno hayo, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi?Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu. Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! Ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

Maoni


Ingia utoe maoni