Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. ANTONI WA PADUA (Jumanne, Juni 13, 2017)
2Kor. 1:18 – 22
Kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Nidyo na siyo. Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Krito, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.
Zab. 119:129 – 133, 135
Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.
(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako.
Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
Unigeukie, unirehemu mimi,
Kama iwahusuvyo walipendao jina lako.
(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako.
Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,
Uovu usije ukanimiliki.
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako.
(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako.
Zab. 19:18
Aleluya, aleluya.
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.
Mt 5:13-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni