Ijumaa. 17 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 6 ya Pasaka (Jumanne, Mei 23, 2017)  

Somo la 1

Mdo. 16:22-34

Siku ile, pale Filipi, wenyeji waliwakamata Paulo na Sila, wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa. Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema, Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani, akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku, akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati huo huo. Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 138; 1-3, 7-8

Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa. au Aleluya.

Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa. au Aleluya.

Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako.
(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa. au Aleluya.

Shangilio

Kol 3:1

Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, amcketi mkono wa kuume wa dunia.
Aleluya.

Injili

Yn 16:5-11

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi? Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.

Maoni


Ingia utoe maoni