Ijumaa. 17 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 6 ya Pasaka (Jumatatu, Mei 22, 2017)  

Somo la 1

Mdo. 16:11-15

Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambave moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.

Wimbo wa Katikati

Zab. 149 :16, 9

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Bwana awaridhia watu wake. au Aleluya.
Au: Aleluya.

Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
(K) Bwana awaridhia watu wake. au Aleluya.
Au: Aleluya.

Watauwa na waushangilic utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote.
(K) Bwana awaridhia watu wake. au Aleluya.
Au: Aleluya.

Shangilio

Rum. 6 : 9

Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka katika wafu hafi tena wala mauti haimtawali tena.
Aleluya.

Injili

Yn. 15:26-16:4

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.

Maoni


Ingia utoe maoni