Masomo ya Misa
Jumatatu ya 5 ya Pasaka (Jumatatu, Mei 15, 2017)
Mdo. 14:5-18
Siku zile, palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe, wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, mji wa Likaonia, na nchi zilizo kando kando; wakakaa huko, wakiihubiri Injili. Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa. Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa, akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda. Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu. Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji. Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng’ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano. Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele, wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi ni wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe. Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha. Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.
Zab. 115 :1-4, 15-16
Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi,
Bali ulitukuze jina lako.
Kwa ajili ya fadhili zako,
Kwa ajili ya uaminifu wako.
Kwa nini mataifa kusema,
Yuko wapi Mungu wao?
(K) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako.
Lakini Mungu wctu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.
(K) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako.
Na mbarikiwe ninyi na Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi.
Mbingu ni mbingu za Bwana,
Bali nchi amewapa wanadamu.
(K) Ee Bwana, kutukuza usitutukuze sisi, Bali ulitukuze jina lako.
Kol. 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu.
Aleluya.
Yn. 14:21-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Maoni
Ingia utoe maoni