Ijumaa. 17 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 4 ya Pasaka (Alhamisi, Mei 11, 2017)  

Somo la 1

Mdo 13:13-25;

Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohane akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa lisemeni. Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa. Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini; baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua DAudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sisitahili kumlegezea viatu vya miguu yake.

Wimbo wa Katikati

Zab. 89:1-2, 20-21, 26-27

Kwa kinywa change
Nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, FAdhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele.

Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
Na mkono wangu utamtia nguvu.
(K) Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele.

Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
(K) Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele.

Shangilio

Yn. 10:27

Aleluya, aleluya.
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, wao wanifuata.
Aleluya.

Injili

Yn. 13:16-20

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa, aliyekula chakula change ameniinulia kisigino chake. Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye. Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu yeyote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yaye aliyenipeleka.

Maoni


Ingia utoe maoni