Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi Kuu (Alhamisi, Aprili 13, 2017)  

Somo la 1

Kut 12:1-8, 11-14

Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni.Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele

Wimbo wa Katikati

Zab 116:12-13, 15-18

Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu;
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K)Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je, !Si ushirika wa damu ya Kristo?

Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako,
Umevifungua vifungo vyangu.
(K)Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je, !Si ushirika wa damu ya Kristo?

Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
Na kulitangaza jina la Bwana;
Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
(K)Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je, !Si ushirika wa damu ya Kristo?

Somo la 2

1Kor 11:23-26

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.

Injili

Yn 13:1-15

Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.

Maoni


Ingia utoe maoni