Masomo ya Misa
Jumanne ya 4 ya Kwaresima (Jumanne, Machi 28, 2017)
Eze. 47:1-9, 12
Malaika alinileta mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraa elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraa elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, Mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisonganamacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko; maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi popote utakapofikilia mto huo. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.
Zab. 46:1-2, 4-5, 7-8
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
(K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,
Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;
Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
(K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Njoni myatazame matendo ya Bwana,
Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
(K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Amo. 5:14
Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi, hivyo Bwana, atakuwa pamoja nanyi.
Yn. 5:1-3, 5-16
Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Betzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza. Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike uende, ni nani? Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maan aYesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.
Maoni
Ingia utoe maoni