Masomo ya Misa
Jumatano ya 3 ya Kwaresima (Jumatano, Machi 22, 2017)
Kumb. 4:1, 5-9
Musa aliwaambia makutano: Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mmzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwmingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.
Zab. 147:12-13, 15-16, 19-20
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapingo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Huipeleka amri yake juu ya nchi,
Neno lake lapiga mbio sana.
Ndiye atoaye theluji kama sufu,
Huimwaga barafu yake kama majivu.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua.
(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.
Shangilio
Mbegu neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu; Yeyote ampataye, ataishi milele.
Mt. 5:17-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msidhani kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni