Masomo ya Misa
Jumatano ya 2 ya Kwaresima (Jumatano, Machi 15, 2017)
Yer 18:18-20
Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.
Zab 31:4-5, 13-15
Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana
Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walifanya hila wauondoe uhai wangu.
(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana
Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.
(K) Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana
Lk. 8:15
Heri wale walishikao neno la Mungu katika moyo wao mwema na unyofu, na wazaao matunda katika uvumilivu.
Mt 20:17-28
Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka. Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu. Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Maoni
Ingia utoe maoni