Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 1 Kwaresima (Jumanne, Machi 07, 2017)  

Somo la 1

Isa. 55:10-11

Bwana asema: Kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko: bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

Wimbo wa Katikati

Zab. 34:3-6, 15-18

Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Wenye haki, Bwana anawaponya na taabu zao zote.

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Wenye haki, Bwana anawaponya na taabu zao zote.

Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
Na masikio yaje hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoa kumbukumbu lao duniani.
(K) Wenye haki, Bwana anawaponya na taabu zao zote.

Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
(K) Wenye haki, Bwana anawaponya na taabu zao zote.

Shangilio

Zab. 95:8

Leo msifanye migumu mioyo yenu, lakini msikie sauti yake Bwana.

Injili

Mt. 6:7-15

Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi: Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

Maoni


Ingia utoe maoni