Masomo ya Misa
Jumatatu ya 8 ya Mwaka (Jumatatu, Februari 27, 2017)
YbS. 17 : 24-29
Hata hivyo huwajalia wale watubuo kurudi, na wao wanaopotewa na saburi kuwafariji. Basi umrudie Bwana na kuacha dhambi; omba dua yako mbele za uso wake na kupunguza kikwazo; umgeukie tena Yeye Aliye juu, uyageue maovu, uyakirihi yaliyo machukizo. Yaani, Mungu anayo ridhaa gani kwao wanaopotea? ila kwao wanaoishi na kumtolea shukrani. Shukrani hukoma kutoka kwa wafu, kama kutoka kwake yeye asiyekuwapo; bali mwenye uzima na afya atamhimidi Bwana, Ee ajabu ya wingi wa rehema za Bwana, na ya masamaha yake kwao wanaomgeukia!
Zab. 12 :1-2,5-7
Heri aliyesamehewa dhambi,
Na kusitiriwa makosa yake.
Heri Bwana asiyemhesabia upotovu.
Ambaye rohoni mwake hamna hila.
(K) Mfurahieni Bwana, shangilieni, enyi wenye haki.
Nalikujulisha dhambi yangu,
Wala sikuuficha upotovu wangu.
Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa Bwana,
Nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu.
(K) Mfurahieni Bwana, shangilieni, enyi wenye haki.
Kwa hiyo kila mtu mtauwa
Akuombe wakati unapopatikana.
Hakika maji makuu yafurikapo,
Hayatamfikia yeye.
Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso,
utanizungusha nyimbo za wokovu.
(K) Mfurahieni Bwana, shangilieni, enyi wenye haki.
Zab. 147:12,15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
Mk. 10:17-27
Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja, Enenda ukauze ulivyo navyo vyote. Uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu, Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maanayoteyawezekana kwa Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni