Masomo ya Misa
Dominika ya 8 ya Mwaka (Jumapili, Februari 26, 2017)
Isa 49:14-15
Sayuni alisema, Yehova ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
Zab 62:1-2, 5-8
Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya,
Wokovu wangu hutoka kwake.
Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
Ngome yangu, sitatikisika sana.
(K) Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya
Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya.
Tumaini langu hutoka kwake.
Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
Ngome yangu, sitatikisika sana.
(K) Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya
Kwa Mungu wokovu wangu, Na utukufu wangu; Mwamba wa nguvu zangu,
Na kimbilio langu ni kwa Mungu.
8 Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake;
Mungu ndiye kimbilio letu.
(K) Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya
1Kor 4:1-5
Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu. Lakini, kwangu mimi, si kitu kabisa nihukumiwe na ninyi, wala kwa hukumu ya kibinadamu, wala sijihukumu hata nafsi yangu. Maana sijui sababu ya kujishitaki nafsi yangu, lakini sihesabiwi haki kwa ajili hiyo; ila anihukumuye mimi ni Bwana. Basi ninyi msihukumu neno kabla ya wakati wake, hata ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo; ndipo kila mtu atakapoipata sifa yake kwa Mungu.
Mt 4:4
Aleluya, aleluya
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya
Mt 6:24-34
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao? Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni