Alhamisi. 19 Septemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 3 ya Kwaresima (Jumanne, Machi 01, 2016)  

Somo la 1

Dan 3:25, 34-43

Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema; Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya Ibrahim umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako, ambao uliwahaidia ya kuwa utawazidishia uzao wao kama nyota za mbinguni na kama mchanga uliopo pwani. Maana sisi, Eye Bwana tumekuwa duni kuliko mataifa mengine yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba, wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema. Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng'ombe, na kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika. Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha na kuufuata uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawa sawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 25:4-9

Ee Bwana, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana Wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.

Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako, Maana zimekuwako tokea zamani.
Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu, Wala maasi yangu. Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako, Ee Bwana kwa ajili ya wema wako.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.

Bwana yu mwema, mwenye adili, Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu, Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.

Injili

Mt 18:21-35

Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

Maoni


Ingia utoe maoni