Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA MT. POLIKARPO (ASKOFU NA SHAHIDI) (Alhamisi, Februari 23, 2017)  

Somo la 1

YbS. 5:1 – 8

Usizitumainie mali zako, wala usiseme, Zanitosha basi. Usifuate roho yako na nguvu zako, kuandamana na tamaa za moyo wako. Usiseme, nani atakayenitawala? Hakika Bwana atakulipiza kisasi. Usiseme, Nalikosa ikanipata nini? Hakika Bwana ndiye mvumilivu. Mintarafu upatanisho, usiwe mjasiri wa kutenda dhambi juu ya dhambi; wala usiseme, Huruma zake zi nyingi. Kwa sababu rehema na ghadhabu zatoka kwake, na hasira yake itawakalia wakosaji. Usichelewe kumrudia Bwana, wala usikawie siku kwa siku; kwa maana ghadhabu ya Bwana itatokea kwa ghafula, nawe utaangamia wakati wa kisasi. Wala usizitegemee mali za udhalimu, kwa kuwa hazitakufaida lolote siku ile ya hasira.

Wimbo wa Katikati

Zab. 1:1 – 4, 6

Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wal ahakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa.
(K) heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea.
(K) heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Shangilio

Zab. 119:105

Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.

Injili

Mk. 9:41-50

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amin, nawaambia, hatakosa thawabu yake. Na yeyote atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, afadhali afungiwe jiwe la kusagia shingoni mwake, na kutupwa baharini. Na mkono wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima u kigutu, kuliko kuwa na mikono miwili, na kwenda zako jehanum, kwenye moto usiozimika; amambo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na mguu wako ukikukosesha, ukate; ni afadhali kuingia katika uzima, u kiwete kuliko kuwa na miguu miwili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Na jicho lako likikukosesha, ling’oe, ulitupe; ni afadhali kuingia katika ufalme wa Mungu, una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum; ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki. Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto. Chumvi ni njema; lakini chumvi ikiwa si chumvi tena, mtaitia nini ikolee? Mwe na chumvi ndani yenu, mkakae kwa amani ninyi kwa ninyi.

Maoni


Ingia utoe maoni