Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 7 ya Mwaka (Jumanne, Februari 21, 2017)  

Somo la 1

YbS. 2:1 – 11

Mwanangu, ukija kumtumikia Bwana, weka tayari roho yako kwa kujaribiwa. Ujitengeneze moyo ustahimili, wala usitaharuki siku ya kuteswa. Uambatane naye wala usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe. Kila utakalopelekewa ulipokee kwa kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako. Maana dhahabu hujaribiwa moto na watu wateule kalibuni mwa unyonge. Basi, umwamini Yeye, naye atakusaidia; ukazinyoshe njia zako, na kulikaza taraja lako katika Yeye. Enyi mnaomcha Bwana, Zingojeeni upande msije mkaanguka. Enyi mnaomcha Bwana, Mwaminini Yeye sana, Thawabu yenu haitawapotea. Enyi mnaomcha Bwana, Sasa tarajieni mema, na furaha ya daima na rehema. Angalieni vizazi vya kale mkaone; Nani aliyemtumaini Bwana akaaibika? Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa? Nani aliyemwita akadharauliwa? Mradi Bwana yu mwenye huruma na rehema, Husamehe dhambi na kuokoa wakati wa shida.

Wimbo wa Katikati

Zab. 37:3 – 4, 18 – 19, 27 – 28, 39 – 40

Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.

Bwana anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hawataaibika wakati wa ubaya,
Na siku za njaa watashiba.
(K) Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.

Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Kwa kuwa Bwana hupenda haki,
Wala hawaachi watauwa wake.
(K) Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.

Na wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa.
(K) Umkabidhi Bwana njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Maagizo yako yote, ee Bwana, ni ambayo yamethibitika milele na milele.
Aleluya.

Injili

Mk. 9: 30 – 37

Yesu na wanafunzi wake wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea motto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.

Maoni


Ingia utoe maoni