Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 7 ya Mwaka (Jumapili, Februari 19, 2017)  

Somo la 1

Law 19:1-2, 17-18

Bwana alinena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 103:1-4, 8, 10, 12-13

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema,
(K) Bwana amejaa huruma na neema

Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
(K) Bwana amejaa huruma na neema

Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
(K) Bwana amejaa huruma na neema

Somo la 2

1Kor 3:16-23

Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi. Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao. Na tena, Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni ya ubatili. Basi, mtu ye yote na asijisifie wanadamu. Kwa maana vyote ni vyenu; kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Shangilio

Yn 14:23

Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda; Nasi tutakuja kwake.
Aleluya

Injili

Mt 5:38-48

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Maoni


Ingia utoe maoni