Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 6 ya Mwaka (Jumamosi, Februari 18, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 11:1 – 7

Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana na mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. Kwa Imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri. Kwa Imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena. Kwa imanai Henoko alihamishwa, asije akaona mauti, wala hakuonekana, kwa sababu Mung alimhamisha: maana kabla ya kuhamishwa alikuwa ameshuhudiwa kwamba amempendeza Mungu. Lakini pasipo Imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. Kwa imanai Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo akauhukumu makosa ulimwengu akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa Imani.

Wimbo wa Katikati

Zab. 145:2 – 5, 10 – 11

Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele.

Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako,
Kitayatangaza matendo yako makuu.
Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako
Na matendo yako yote ya ajabu.
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele.

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
(K) Ee Bwana, nitalihimidi jina lako milele.

Shangilio

Zab. 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.

Injili

Mk. 9:2 – 13

Siku ile Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane, akawaleta juu yam lima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizruri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao. Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza na kurejeza upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.

Maoni


Ingia utoe maoni