Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 6 ya Mwaka A (Jumapili, Februari 12, 2017)  

Somo la 1

Ybs 15:15-20

Ukipenda utazishika amri zake, na kutenda amini ni shauri lako. Ameweka mbele yako moto na maji; utanyosha mkono wako uchaguavyo. Mbele ya mwanadamu upo uzima na mauti, naye atapewa apendavyo. Mradi hekima ya Bwana yatosha, mkuu mwenye uweza hutazama vyote, Macho yake ni juu yao wamchao, naye atapeleleza kila kazi ya watu. Hakumwamuru mtu yeyote awe asi, wala kumruhusu atende dhambi.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:1-2, 4-5, 17-18, 33-34

Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti,
Nizitii amri zako.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako,
Nami nitaishika hata mwisho.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Somo la 2

1 Kor 2:6-10

Ndugu zangu, walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu; lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

Shangilio

Yn. 14:6

Aleluya, aleluya.
Mimi ndimi Njia, na Ukweli, na Uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

Injili

Mt 5:17-37

Yesu aliwaambia wanafunzi wake ; Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho. Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini. Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako; lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.

Maoni


Ingia utoe maoni