Jumapili. 19 Mei. 2024

Masomo ya Misa

SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI (Alhamisi, Februari 02, 2017)  

Somo la 1

Mal. 3:1-4

Bwana Mungu asema hivi: Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi. Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo; naye ataketi kama asafishaye fedha na kuitakasa, naye atawatakasa wana wa Lawi, atawasafisha kama dhahabu na fedha; nao watamtolea Bwana dhabihu katika haki. Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani.

Wimbo wa Katikati

Zab. 24:7-10

Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Inukeni, enyi malango ya milele,
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani Mfalme wa utukufu? Ni Bwana.


Ni nani Mfalme wa utukufu?
Bwana mwenye nguvu, hodari,
Bwana hodari wa vita.
(K) Ni nani Mfalme wa utukufu? Ni Bwana.


Inueni vichwa vyenu, enyi malango,
Naam, viinueni, enyi malango ya milele
Mfalme wa utukufu apate kuingia.
(K) Ni nani Mfalme wa utukufu? Ni Bwana.


Ni nani huyu Mfalme wa utukufu?
Bwana wa majeshi,
Yeye ndiye Mfalme wa utukufu.
(K) Ni nani Mfalme wa utukufu? Ni Bwana.

Somo la 2

Ebr. 2:14-18

Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi, awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa. Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu. Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.

Shangilio

Lk. 2:32

Aleluya, aleluya!
Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.
Aleluya!

Injili

Lk. 2:22-40

Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, wazee wa Yesu walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Huwa wawili au makinda ya njiwa wawili. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mkononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, kwa amani, kama ulivyosema; kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, uliouweka tayari machoni pa watu wote; nuru ya kuwa mwangaza wa mataifa, na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

Maoni


Ingia utoe maoni