Jumapili. 19 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 4 ya Mwaka (Ijumaa, Februari 03, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 13:1 – 8

Upendano wa ndugu na udumu. Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua. Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mliavyo katika mwili. Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye ymwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini? Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni Imani yao. Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

Wimbo wa Katikati

Zab. 27:1, 3, 5, 8 – 9

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani?
Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
Moyo wangu hautaogopa.
Vita vijaponitokea
Hata hapo nitatumaini.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya,
Atanisitiri katika sitara ya hema yake,
Na kuniinua juu ya mwamba.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako,
Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu usinitupe.
(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

Shangilio

Zab. 130:5

Aleluya, aleluya,
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.

Injili

Mk. 6:14-29

Mfalme Herode alisikia habari; kwa maana jina lake lilikuwa kutangaa, akasema, Yohane Mbatizaji amefufuka katika wafu, na kwa hiyo nguvu hizi zinatenda kazi ndani yake. Wengine walisema, Ni Eliya. Wengine walisema, Huyu ni nabii, au ni kama mmoja wa manabii. Lakini Herode aliposikia, alisema, Yohane mwenyewe alikuwa amefufuka. Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohane, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake; kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohane alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohane; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lolote utakalo nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohane Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi, akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Maoni


Ingia utoe maoni