Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 3 ya Mwaka (Ijumaa, Januari 27, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 10:32 – 39

Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wetu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa Imani; naye akisitasita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na Imani ya kutuokoa roho zetu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 37:3 – 6, 23 – 24, 39 – 40

Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Umkabidhi Bwana njia yako pia umtumaini
Naye atafanya;
Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake.
Ajapojikwaa hataanguka chini,
Bwana humshika mkono na kumtegemeza.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Wokovu wa wenye haki una Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

Shangilio

1Thes. 2:13

Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.

Injili

Mk. 4:26-34

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.

Maoni


Ingia utoe maoni