Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA MT. THOMAS WA AKWINO (Jumamosi, Januari 28, 2017)  

Somo la 1

Ebr. 11:1 – 2, 8 – 19

Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana. Maana kwa hiyo wazee wetu walishuhudiwa. Kwa Imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopata kuwa urithi; akatoka asijue aendako. Kwa Imani alikaa nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi, ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu. Kwa Imani hata Sara mwenyewe alipokea uwezo wa kuwa na mimba, alipokuwa amepita wakati wake, kwa kuwa alimhesabu yeye aliyeahidi kuwa mwaminifu. Na kwa ajili ya hayo wakazaliwa na mtu mmoja, naye alikuwa kama mfu, watu wengi kama nyota za mbinguni wingi wao, na kama mchanga ulio ufuoni, usioweza kuhesabika. Hawa wote wakafa katika Imani, wasijazipokea zile ahadi bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi. Maana hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. Na kama wangaliikumbuka nchi ile waliyotoka, wangalipa nafsi ya kurejea. Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni haya kuitwa Mungu wao; maana amewatengenezea mji. Kwa Imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanwe, mzaliwa pekee; Naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.

Wimbo wa Katikati

Lk. 1:69 – 75

Ametusimamishia pembe ya wokovu
Katika mlango wa Daudi mtumishi wake.
Kama alivyosema tangu mwanzo
Kwa kinywa cha manabii wake watakatifu.
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake.


Tuokolewe na adui zetu
Na mikononi mwao wote wanaotuchukia:
Ili kuwatendea rehema baba zetu,
Na kulikumbuka agano lake takatifu.
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake.

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote.
(K) Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, kwa kuwa amewajia watu wake.

Shangilio

Yn. 14:23

Aleluya, aleluya,
Mtu akinipenda, atalishika neno langu, na baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya.

Injili

Mk. 4:35-41

Siku ile kulipokuwa jioni, Yesu akawambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo. Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwako pamoja naye. Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna Imani bado? Wakaingiwa na hofu kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?

Maoni


Ingia utoe maoni