Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA WATAKATIFU TIMOTHEO NA TITO, MAASKOF (Alhamisi, Januari 26, 2017)  

Somo la 1

2 Tim. 1:1-8

Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa ajili ya ahadi ya uzima ulio katika Kristo Yesu; kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Namshukuru Mungu, nimwabuduye kwa dhamiri safi tangu zamani za wazee wangu, kama vile nikukumbukavyo wewe daima, katika kuomba kwangu usiku na mchana. Nami natamani sana kukuona, nikiyakumbuka machozi yako, ili nijae furaha; nikiikumbuka Imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo. Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yao kwa kuwekewa mikono yangu. Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu nay a upendo nay a moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 16:1-2, 5, 7-8, 11

Mungu, unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu,
Sina wema ila utokao kwako.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Utanijulisha njia ya uzima,
Mbele za uso wako iko furaha tele,
Na katika mkono wako wa kuume
Mna mema ya milele
(K) Bwana ndiye fungu la posho langu.

Shangilio

Mt. 28:19-20

Aleluya, aleluya,
Enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, Bwana anasema. Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Aleluya.

Injili

Lk. 10:1-9

Bwana aliweka wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni; angalieni, nawatuma kama wana-kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.

Maoni


Ingia utoe maoni