Masomo ya Misa
Jumatatu 3 ya Mwaka (Jumatatu, Januari 23, 2017)
Ebr. 9:15, 24 – 28
Kristo ni mjumbe wa agano jipya, ili, mauti ikiisha kufanyika kwa kukomboa makosa yaliyokuwa chini ya agano la kwanza, hao walioitwa waipokee ahadi ya urithi wa milele. Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu, lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.
Zab. 98:1 – 6
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi;
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele ya mfalme, Bwana.
(K) Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
2Tim. 1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristu alibatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika kwa Injili.
Aleluya.
Mk. 3:22-30
Waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo. Yesu akawaita akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani? Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama; na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama. Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo. Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake. Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote; bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakauwa ana dhambi ya milele; kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.
Maoni
Ingia utoe maoni