Alhamisi. 31 Julai. 2025

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Watakatifu Martha, Mariamu na Lazaro (Jumanne, Julai 29, 2025)  

Somo la 1

1Yoh 4:7-16

Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu. Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.

Wimbo wa Katikati

Zab 34: 2-11

Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.
(K) Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.
Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
(K) Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
(K) Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

Wana-simba hutindikiwa, huona njaa;
Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
(K) Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.

Injili

Yn 11:19-27

Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

Maoni


Ingia utoe maoni