Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya 2 ya Noeli (Alhamisi, Januari 05, 2017)  

Somo la 1

1 Yn 3:11-21

Wapenzi: Hii ndiyo habari mliyoisikia tangu mwanzo, kwamba tupendane sisi kwa sisi; si kama Kaini alivyokuwa wa yule mwovu, akamwua ndugu yake. Naye alimwua kwa sababu gani? Kwa sababu matendo yake yalikuwa mabaya, na ya ndugu yake yalikuwa ya haki. Ndugu zangu, msistaajabu, ulimwengu ukiwachukia. Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti. Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je! Upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu;

Wimbo wa Katikati

Zab 100

Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;
(K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote

Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
(K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote

Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake;
(K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote

Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
(K) Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote

Shangilio

Ebr. 1:1-2

Aleluya, aleluya,
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi, na kwa namna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, Siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.

Injili

Yn 1:43-51

Siku ile, Yesu alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate. Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro. Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone. Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Maoni


Ingia utoe maoni