Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Mt. Stephano Shahidi na Mtume (Jumatatu, Desemba 26, 2016)  

Somo la 1

Mdo 6:8-10: 7:54-60

Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.

Wimbo wa Katikati

Zab 31:2-3, 5-7, 16, 20

Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
Nyumba yenye maboma ya kuniokoa.
Ndiwe genge langu na ngome yangu;
Kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge.
(K)Mikononi mwako, naiweka roho yangu, Ee Bwana

Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako,
(K)Mikononi mwako, naiweka roho yangu, Ee Bwana

Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.
(K)Mikononi mwako, naiweka roho yangu, Ee Bwana

Injili

Mt 10:17-22

Yesu aliwaambia mitume wake: Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.

Maoni


Ingia utoe maoni