Masomo ya Misa
Alhamisi ya 4 ya Majilio (Alhamisi, Desemba 22, 2016)
1 Sam 1:24-28
Siku zile, Hana alimchukua pamoja naye, na ng'ombe watatu, na efa moja ya unga,na chupa ya divai,akamleta nyumbani kwa BWANA,huko Shilo ;na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo. Nao wakamchinja huyo ng'ombe, wakamleta mtoto kwa Eli. Akasema, Ee bwana wangu, kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mimi ndimi yule mwanamke aliyesimama karibu nawe hapa, nikimwomba Bwana. Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko.
1 Sam: 2:1, 4-8
Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia Bwana,
Pembe yangu imetukuka katika Bwana,
Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu;
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.
Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.
Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.
Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba,
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.
Bwana huua, naye hufanya kuwa hai;
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.
Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.
Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,
Ili awaketishe pamoja na wakuu,
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;
Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana,
Naye ameuweka ulimwengu juu yake.
(K) Moyo wangu wamshangilia Bwana mwokozi wangu.
Shangilio
Aleluya, aleluya,
Ee Mfalme wa mataifa na jiwe la msingi wa Kanisa uje kumwokoa mwanadamu aliyemuumba kwa udongo.
Aleluya.
Lk 1:46-56
Siku ile Mariamu alisema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi Kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.
Maoni
Ingia utoe maoni