Ijumaa. 03 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 3 ya Majilio (Jumanne, Desemba 13, 2016)  

Somo la 1

Sef 3:1-2, 9-13

Bwana asema: Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu! Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini Bwana; hakumkaribia Mungu wake. Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la Bwana, wamtumikie kwa nia moja. Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu. Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana. Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.

Wimbo wa Katikati

Zab 34:1-2, 5-6, 16-17, 18, 22

Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia

Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia

Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
Walilia, naye Bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia

Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
(K) Maskini aliita, Bwana akasikia

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Uje, Bwana, wala usikawie; Uzisamehe dhambi za taifa lako.
Aleluya.

Injili

Mt 21:28-32

Siku ile Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee: Mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu. Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende. Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda. Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

Maoni


Ingia utoe maoni