Alhamisi. 26 Desemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 1 ya Majilio (Jumapili, Desemba 01, 2024)  

Somo la 1

Yer 33:14-16

Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda. Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii. Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.

Wimbo wa Katikati

Zab 25:4-5, 8-9,10,14

Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli,
Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake.
Siri ya Bwana iko kwao wamchao.
Naye atawajulisha agano lake.
(K) Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu.

Somo la 2

1Thes 3:12; 4:1-2

Ndugu zangu; Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote. Iliyobaki, ndugu, tunakusihi na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu.

Shangilio

Zab 85:7

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana utuonyeshe rehema zako, Utupe wokovu wako.
Aleluya.

Injili

Lk 21:25-28, 34-36

Siku ile kutakuwa ishara katika jua; na mwezi na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake; watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazama mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika. Hapo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika wingu pamoja na nguvu na utukufu mwingi. Basi, mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia. Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafla, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.

Maoni

DAVID ELIA

Amina!

Ingia utoe maoni