Alhamisi. 26 Desemba. 2024

Masomo ya Misa

SHEREHE YA BWANA WETU YESU KRISTU MFALME (Jumapili, Novemba 24, 2024)  

Somo la 1

Dan 7:13-14

Niliona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 93:1-2,5

Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.
(K) Bwana ni mfalme, amejivika taji.

Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani.
Wewe ndiye uliye tangu milele.
(K) Bwana ni mfalme, amejivika taji.

Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako.
Ee Bwana, milele na milele.
(K) Bwana ni mfalme, amejivika taji.

Somo la 2

Ufu. 1:5-8

Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam, Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.

Shangilio

Mk 11:10

Aleluya, aleluya!
Abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana; Ubarikiwe na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi.
Aleluya.

Injili

Yn 18:33-37

Pilato aliingia ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia: Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu? Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.

Maoni

Sabas Salvatory Kazule

Ufalme wetu na uongozi wetu, uwe kama wa bwana wetu yesu kristo

Ingia utoe maoni