Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mtakatifu Sesilia, Bikira na Shahidi (Ijumaa, Novemba 22, 2024)  

Somo la 1

Ufu 10:8–11

Mimi, Yohane, nilisikia sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, ukakitwae kile kitabu kilichofunguliwa katika mkono wa yule malaika, aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi. Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. Wakaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131

Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
Kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.

Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asalai kinywani mwangu.
(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.

Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
(K) Mausia yako ni matamu sana kwangu.

Shangilio

2Kor 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristu, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.

Injili

Lk 19:45-48

Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara, akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi. Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza; wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.

Maoni


Ingia utoe maoni