Ijumaa. 03 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 3 ya Majilio (Jumapili, Desemba 11, 2016)  

Somo la 1

Isa 35:1-6, 10

Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.

Wimbo wa Katikati

Zab 146:6-10

Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa;
(K) Uje Bwana kutuokoa

Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni;
(K) Uje Bwana kutuokoa

Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele, Mungu wako,
Ee Sayuni, kizazi hata kizazi.
(K) Uje Bwana kutuokoa

Somo la 2

Yak 5:7-10

Ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni, mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.

Shangilio

Lk 4:18

Aleluya, aleluya
Roho wa Bwana yu juu yangu, Amenituma kuwahubiri maskini habari njema;
Aleluya

Injili

Mt 11:2-11

Siku ile, Yohane aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine? Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami. Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohane, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye.

Maoni


Ingia utoe maoni