Ijumaa. 03 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 2 ya Majilio (Jumamosi, Desemba 10, 2016)  

Somo la 1

Ybs 48:1-4,9-11

Ndipo aliposimama nabii Eliya, kaka moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao, na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto. Jinsi ulivyotisha kwa miujiza yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Akachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli. Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.

Wimbo wa Katikati

Zab 80: 1-2, 14-15, 17-18

Wewe uchungaye Israeli, usikie,
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako.
(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe, Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya Kuwa imara kwa nafsi yako.
(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe, Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.

Mkono wako na uwe juu yake Mtu wa mkono wako wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
(K) Ee Bwana Mungu wetu, uturudishe, Utuangazishe uso wako, nasi tutaokoka.

Shangilio

Lk. 3:4,6

Aleluya, aleluya,
Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,
Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,
Aleluya.

Injili

Mt 17:10-13

Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani: Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote, ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao. Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohane Mbatizaji.

Maoni


Ingia utoe maoni