Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 31 ya Mwaka (Jumanne, Novemba 05, 2024)  

Somo la 1

Flp 2:5-11

Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

Wimbo wa Katikati

Zab 22:25-31

Nitaziondoa nadhiri zangu
Mbele yao wamchao.
Wapole watakula na kushiba,
Wamtafutao Bwana watamsifu;
Mioyo yenu na iishi milele.
(K) Kwako zinatoka sifa zangu, Ee Bwana.

Miisho yote ya dunia itakumbuka,
Na watu watamrejea Bwana;
Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
Maana ufalme una Bwana,
Naye ndiye awatawalaye mataifa.
Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu.
(K) Kwako zinatoka sifa zangu, Ee Bwana.

Wazao wake watamtumikia.
Zitasimuliwa habari za Bwana,
Kwa kizazi kitakachokuja,
Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
Ya kwamba ndiye aliyeyafanya.
(K) Kwako zinatoka sifa zangu, Ee Bwana.

Shangilio

Mt 4:4

Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.
Aleluya.

Injili

Lk 14:15-24

Mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja na Yesu alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu. Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi, akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari. Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya miji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete. Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, n ahata sasa ingaliko nafasi. Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa. Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.

Maoni


Ingia utoe maoni