Masomo ya Misa
Dominika ya 31 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 03, 2024)
Kumb 6:2-6
Musa aliwaambia makutano: Upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zoko ziongezwe. Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako.
Zab 18:1-3,46,50
Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu,
Na boma langu na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayekukimbilia.
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu,
Na ngome yangu.
Nitamwita Bwana anayestahili kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
(K) Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana.
Bwana ndiye aliye hai,
Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu
Ampa mfalme wake wokovu mkuu,
Amfanyia fadhili masihi wake.
(K) Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana.
Ebr 7:23-28
Wale walifanywa makuhani wengi, kwa sababu wazuiliwa na watu wasikae; bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee. Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lolote, aliyetengewa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi zao hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake. Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele.
Yn 15:28-34
Aleuya, aleluya.
Ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Mk 12:28-34
Mmojawapo wa waandishi alifika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja, nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.
Maoni
Edmond Wafula
Tumshukuru MunguIngia utoe maoni