Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 30 ya Mwaka (Jumanne, Oktoba 29, 2024)  

Somo la 1

Efe 5:21–33

Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa atukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wal alolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda wenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye navyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

Wimbo wa Katikati

Zab 128:1–5

Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako.
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

Shangilio

1Pet 1:25

Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.

Injili

Lk 13:18-21

Yesu alisema, Ufalme wa Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punji ya haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa angani wakakaa katika matawi yake. Akasema mara ya pili, Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke akaisitiri ndani ya pichi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.

Maoni


Ingia utoe maoni