Masomo ya Misa
Ijumaa ya 27 ya Mwaka (Ijumaa, Oktoba 11, 2024)
Gal 3:7-14
Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani. Kwa maana wale walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye. Ni Dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani. Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba Baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristu, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
Zab 111:1-6
Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu,
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
(K) Alikumbuka agano lake milele.
Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu,
Bwana ni mwenye fadhili na rehema.
(K) Alikumbuka agano lake milele.
Amewapa wamchao chakula,
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa.
(K) Alikumbuka agano lake milele.
1Sam 3:9, Yn 6:68
Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia; wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
Lk 11:15-26
Wengine wa makutano walisema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo. Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia. Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu aliyekusanya pamoja nami hutawanya. Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitarudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.
Maoni
Ingia utoe maoni