Ijumaa. 17 Mei. 2024

Masomo ya Misa

SIKUKUU YA UKULU WA MT. PETRO (MTUME) (Jumatatu, Februari 22, 2016)  

Somo la 1

1 Pet. 5:1-4

Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu ile isiyokauka.

Wimbo wa Katikati

Zab. 23 (K) 1



Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

Huniuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.
(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.

Injili

Mt. 16:13-19

Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni