Masomo ya Misa
Jumanne ya 25 ya Mwaka (Jumanne, Septemba 24, 2024)
Mit 21:1–6, 10–13
Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; kama mfereji wa maji huugeuza popote apendapo. Kila njia ya mtu ni sawa machoni pake mwenyewe; bali Bwana huipima mioyo. Kutenda haki na hukumu humpendeza Bwana kuliko kutoa sadaka. Macho yenye kiburi, na moyo wa kutakabari, hata ukulima wa waovu, ni dhambi. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu; bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Kupata akiba ya mali kwa ulimi wa uongo ni moshi upeperushwao; ni kutafuta mauti. Nafsi ya mtu mbaya hutamani maovu; jirani yake hapati fadhili machoni pake. Mwenye mzaha aadhibiwapo, mjinga hupata hekima; na mwenye hekima afundishwapo, hupokea maarifa. Mwenye haki huitafakari nyumba ya mtu mbaya; jinsi wabaya waangushwavyo wakaangamia. Azibaye masikio yake asisikie kilio cha maskini, yeye naye atalia, lakini hatasikiwa.
Zab 119:1, 27, 30, 34–35, 44
Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Unifahamishe njia ya mausia yako,
Nami nitayatafakari maajabu yako.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
Nimeichagua njia ya uaminifu,
Na kuziweka hukumu zako mbele yangu.
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
Naam, nitaitii kwa moyo wangu wote.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako,
Kwa maana nimependezwa nayo.
Nami nitaitii sheria yako daima,
Naam, milele na milele.
(K) Uniendeshe katika mapito ya maagizo yako, Ee Bwana.
1Pet 1:25
Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.
Lk 8:19–21
Walimwendea Yesu mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Maoni
Ingia utoe maoni