Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Pio wa Pietrelcina, Padre (Jumatatu, Septemba 23, 2024)  

Somo la 1

Mit 3:27–34

Mwanangu, Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda. Usimwambie jirani yako, nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; nawe unacho kitu kile karibu nawe. Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama. Usishindane na mtu bila sababu, ikiwa hakukudhuru kwa lolote. Usimhusudu mtu mwenye jeuri, wala usiichague mojawapo ya njia zake. Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, bali siri yake ni pamoja na wanyofu. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, bali huibariki maskani ya wenye haki. Hakika yake huwadharau wenye dharau, bali huwapa wanyenyekevu neema.

Wimbo wa Katikati

Zab 15

Ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu.
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake
Asiyesingizia kwa ulimi wake.
(K) Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake, katika kilima chako kitakatifu.


Asiyemtendea mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
Ingawa ameapa kwa hasara yake,
Hayabadili maneno yake.
(K) Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake, katika kilima chako kitakatifu.


Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele.
(K) Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake, katika kilima chako kitakatifu.

Shangilio

Yak 1:18

Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.

Injili

Lk 8:16–18

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.

Maoni


Ingia utoe maoni