Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Wat. Andrea Kim Padre, Paulo Chong na Wenzake Mashahidi (Ijumaa, Septemba 20, 2024)
1Kor 15:12–20
Ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu? Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka; tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwenu ni bure na Imani yetu ni bure. Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi. Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka. Na kama Kristo hakufufuka, Imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu. Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea. Kama katika maisha haya tu tumemtumaini Kristo, sisi tu maskini kuliko watu wote. Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.
Zab 17:1, 6–8, 15
Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao wanaowaondokea.
(K) Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako.
Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
Bali mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
(K) Nishibishwe, Ee Bwana, kwa sura yako.
Efe 1:17, 18
Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
Lk 8:1–3
Yesu alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, na Yohana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.
Maoni
Ingia utoe maoni