Jumanne. 22 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 24 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 15, 2024)  

Somo la 1

Isa 50:5-9

Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala siku mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

Wimbo wa Katikati

Zab 116:1-6, 8-9

Aleluya,
Nampenda Bwana kwa kuwa ananisikiliza
Sauti yangu na dua zangu.
Kwa maana amenitegea sikio lake,
Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote!
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.

Kamba za mauti zilinizunguka,
Shida za kuzimu zilinipata.
Niliona taabu na huzuni,
Nikaliitia jina la Bwana;
Ee Bwana, Mungu wangu, uniokoe.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.

Bwana ni mwenye neema na haki,
Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema,
Bwana huwalinda wasio na hila,
Nilikuwa taabuni, akaniokoa.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.

Maana ameniponya nafsi yangu na mauti,
Macho yangu na machozi,
Na miguu yangu na kuanguka.
Nitaenenda mbele za Bwana
Katika nchi za walio hai.
(K) Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi ya walio hai.

Somo la 2

Yak 2:14-18

Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moteo na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.

Shangilio

Mdo 16:14

Aleluya, aleluya.
Fungua mioyo yetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.

Injili

Mk 8:27-35

Yesu alitoka na wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisara Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, Watu huninena mimi kuwa ni nani? Wakamjibu, Yohana Mbatizaji; wengine, Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza huwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu; Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu. Akawaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponywa nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha.

Maoni


Ingia utoe maoni